Bondia wa ngumi za kulipwa Mfaume Mfaume, amesema hatowaangusha mashabiki wake na anajipanga kushinda katika pambano la ‘Usiku wa Vitasa’ litakalofanyika Juni 30, mwaka huu, Dar es salaam.
Mfaume atapanda ulingoni kuzichapa na Nkululeko Mhlongo kutoka Afrika Kusini, katika pambano la uzito wa kati la raundi nane lisilo na ubingwa.
Mfaume amesema ameanza kufanya mazoezi makali kujiandaa na pambano hilo ambalo anaamini atashinda katika raundi za mapema.
Mfaume amesema ana uhakika wa kushinda pambano hilo na kuweka rekodi ya kuendelea kufanya vyema katika mapambano ya kimataifa mwaka huu.
“Ushindi ndio kauli mbiu yangu kila nikiamka, nafanya mazoezi kwa bidii huku nikiwa na lengo la kufanya vyema katika pambano dhidi ya Mhlongo, sitakubali kupigwa katika ardhi ya nyumbani,” alitamba Mfaume.
Promota wa pambano, Fadhili Maogola, amesema maandalizi yameanza huku mabondia wengine watakaopanda ulingoni wakithibitisha kuzichapa.
Amesema pamoja na Mfaume, mabondia wengine wenye rekodi kali watazichapa akiwemo Selemani Kidunda atakayepimana ubavu na Eric Mukadi kutoka DRC.
Maogola amesema Kidunda na Mukadi watawania mkanda ambao utatangazwa baadae.
Mfaume atashuka ulingoni akiwa na kumbukumbu ya kumchakaza kwa KO Abdulmonem Said kutoka Misri, katika pambano lililofanyika mwaka jana jijini Dar es salaam.