Aliyekuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Young Africans ambaye sasa ni Mkurugenzi wa fedha, Haji Mfikirwa amesema jambo kubwa lililodhamiriwa klabuni hapo msimu huu 2021/22, ni kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, baada ya kutoka kapa miaka minne mfululizo.
Young Africans imekua kwenye msako mkali wa kutwaa taji la Ligi kuu tangu mwaka 2017, huku taji hilo likienda Msimbazi yalipo makao makuu ya watani zao wa jadi Simba SC.
Mfikirwa amesema: “Miongoni mwa sera za klabu yetu katika kuwapa motisha wachezaji ni kuhakikisha kunakuwepo na kiwango fulani cha bonasi kwa kila matokeo mazuri wanayoyapata, lakini nikuhakikishie kuwa hicho siyo kitu pekee kinachowapa motisha.
“Motisha kubwa ambayo wachezaji wote wa Yanga wanayo msimu huu ni ile ya kutaka kuandika rekodi ya kuwa sehemu ya kikosi kitakachorejesha ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kupita misimu minne mfululizo bila taji hilo, kila mchezaji anatamani kuona hilo linatimia ndiyo maana wanapambana kufanya vizuri.”
Young Africans imeuanza kwa kasi msimu huu 2021/22 kwa kushinda taji la Ngao ya Jamii na kuvuna alama sita katika michezo yao miwili ya kwanza dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold FC.
Kwa sasa klabu hiyo inakamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikitanguliwa na Polisi Tanzania yenye alama sita, lakini inaongoza kwa mabao ya kufunga.
Mara ya mwisho Young Africans kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ilikuwa msimu wa 2016/17, na baada ya hapo Simba SC ilitwaa taji hilo mara nne mfululizo.