Kutokana na ongezeko kubwa la wanyamapori, Serikali imesema inaimarisha mifumo itakayozuia wanyama hao kuingia katika makazi ya wananchi, ili waweze kuishi kwa amani.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni jijini Dodoma hii leo Juni 9, 2022 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mlalo Rashidi Shangazi.
“Serikali inawajibu wa kulinda mali na usalama wa raia ndani ya nchi na tayari tumeongeza idadi ya askari wa wanyamapori ambao tunawapeleka kwenye mbuga zilizo karibu na makazi ya watu.”
Katika swali lake, Mbunge Shangazi alihoji ni kwa kiasi gani Serikali itawahakikishia usalama wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi hizo ili wasiendelee kupata athari kutokana na uvamizi wa wanyama.
Akiendelea kujibu swali hilo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema jitihada zingine ni pamoja na kuimarisha na kujenga vituo vya kuhifadhia silaha ili kusaidia kuwaondoa wanyama hao na kuwarudisha hifadhini.
“Kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaratibu ujenzi wa vituo 32 vya kuhifadhia silaha kandokando ya maeneo yanayopakana na hifadhi za wanyamapori nah ii itasaidia kuondoa hatari zilizokuwepo awali,” amesema Majaliwa.
Akijibu swali la Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamoga aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wananchi wanaosafiri Ziwa Tanganyika na Nyasa wanapewa usafiri salama, Waziri Mkuu amesema wanafanya jitihada za kuimarisha usafiri katika maeneo ya maziwa na bahari kuu.
“Wote ni mashahidi jitihada za ujenzi wa meli kwenye maeneo hayo zinaendelea na mwanzoni mwa mwaka huu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, alikuwa mkoani Mwanza kushuhudia utiaji saini wa ujenzi wa meli za Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa,” amefafanua Waziri Mkuu.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imefanyia ukarabati meli na vivuko kwenye maeneo matatu ya Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.