Klabu ya Young Africans imebadili mfumo wa kutoa Bonasi kwa wachezaji pindi timu yao inaposhinda ama kutoka sare kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2020/21.

Msimu uliopita Young Africans kwa kushirikiana na wadhamini wao Kampuni ya GSM walikua wanatoa Bonasi kwa wachezaji ya shilingi milioni 10, kwa kila mchezo wanaopata ushindi, ili kuongeza morari kwa wachezaji.

Msimu huu wadhamini Kampuni ya GSM na uongozi wa klabu hiyo wametambulisha mfumo mpya wa utoaji wa Bonasi kwa wachezaji wao, huku dhamira kubwa ikiwa ni kufikia melngo ya kurejesha heshima ya kutwaa taji la VPL, linalomilikiwa na Simba SC kwa msimu mitatu mfululizo.

Akizungumza kupitia kipindi cha michezo cha Mshike Mshike kinachorushwa na Azam TV, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM Hersi Said amesema, mpango mkubwa ni kuona wanaendelea kutoa Bonasi kwa mtindo wa kipekee tofauti na msimu uliopita.

“Msimu uliopita tulikuwa na bonasi katika kila mchezo, wachezaji walikuwa wakishinda basi tunawapa Bonasi, ila wakipoteza na kutoka sare tulikuwa hatutoi Bonasi, msimu huu tunataka kugawa kutokana na pointi ambazo tutakuwa tunazitaka kwamba katika pointi 15 tunazitafuta pointi.

“Lengo ni kuona kwamba katika pointi 15 ikitokea tukapata pointi 10 hapo hela itatolewa na tukipata pointi tano nje ya pointi 15 hapo hakuna sababu ya kupata kitu chochote,” amesema Hersi.

Young Africans tayari imeshacheza michezo miwili ya Ligi Kuu msimu huu, wakianza dhidi ya Tanzania Prisons ambapo walipata matokeo ya sare ya bao moja kwa moja, kisha wakaifunga Mbeya City FC bao moja kwa sifuri.

Mwishoni mwa juma hili Young Africans watacheza mchezo wa mzunguuko watatu dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera.

Biashara Utd kazi wanayo, Manara asema mazito
TANZIA: ACP Jonathan Shana afariki dunia