Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres kupitia hotuba yake kwenye hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa kilele wa muafaka mpya wa kifedha duniani, amerelea ombi lake la mageuzi makubwa ya mfumo wa fedha wa kimataifa ambao hauendani na changamoto zilizopo.
Guterres, ameyasema hayo na kuongeza kuwa Mataifa mengi ya Afrika yanatumia zaidi ulipaji wa deni kuliko katika huduma za afya zinazohitajika sana, na kwamba zaidi ya nchi 50 hazijalipa madeni au zinakaribia hatari ya kutolipa.
Aidha, amekosoa jinsi fedha zinavyotengwa akisema Muungano wa Ulaya ulipokea dola bilioni 160 huku Afrika ikiambulia bilioni 34 huku akibainisha kuwa Raia wa Ulaya anapokea kwa wastani karibu mara 13 zaidi ya raia wa Afrika na kudai kuwa taratibu zinafanyika lakini hazina usawa.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuwepo kwa utaratibu wa msamaha wa deni ambao unaunga mkono kusimamishwa kwa malipo, masharti ya muda mrefu ya kukopesha na viwango vya chini vya riba, ili kufanya ukopaji kuwa nafuu zaidi kwa mataifa maskini.