Serikali imesema ipo mbioni kuanzisha mfumo wa utambuzi na usajili wa barabara zote nchini, hatua inayolenga kuziwezesha barabara zote kujengwa katika viwango vinavyofafana na ubora wa huduma ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi hususani wa maeneo ya vijijini.
Hayo yamesemwa leo wilayani Handeni mkoani Tanga na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara katika Wilaya za Handeni, Kilindi na Korogwe.
Kwandikwa alisema ili kutekeleza adhima hiyo, Serikali imekusudia kuiwezesha Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kwa kuiongezea uwezo wa vitendea kazi na waatalamu wa kutosha ili kuhakikisha kuwa miradi ya barabara iliyopo katika halmashauri zote nchini inakuwa na chombo maalum cha usimamizi.
“Ni wajibu wa watendaji wote kushirikiana katika kusimamia miradi ya barabara, kwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa TARURA ikiwemo kuipata fedha pale inapokwama katika kutekeleza wajibu wake hususani katika maeneo korofi yanayohitaji fedha maalum,” alisema Kwandikwa.
Alisema kukamilika kwa miradi ya barabara katika maeneo mengi ya vijijini kutawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uzalishaji na usafirishaji wa mazao na pembejeo na hivyo kuvutia uwekezaji katika miradi mikubwa ya maendeleo.
Aidha Kwandikwa alisema ili kutekeleza vyema majukumu yake, ni wajibu pia wa TARURA kujisogeza karibu zaidi kwa jamii ikiwemo kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi na viongozi mbalimbali katika Mamlaka ya Serikali za mitaa, hatua inayolenga kujenga uelewa wa mamlaka, wajibu na majukumu ya taasisi hiyo.
Aliongeza kuwa asilimia 80 ya uwezeshaji wa uchumi katika maeneo ya vijijini unategemea upatikanaji wa miundombinu ya barabara za uhakika, hivyo ni wajibu wa TARURA kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kuinua uchumi pasipo kukabiliwa na changamoto zisizo na ulazima.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe alisema wilaya yake imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha kuwa sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinafuatwa katika usimamizi wa miundombinu ya barabara kwa kuwa hatua itasaidia kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi.
“Wilaya imejipanga kikamilifu katika kusimamia sheria ikiwemo kudhibiti mifugo inayovuka kutoka upande mmoja wa barabara kwenda mwingine, kwa kuwa mara nyingi imekuwa ikichangia uharibifu wa miundombinu ya barabara zetu” alisema Gondwe.