Mfumuko wa bei wa taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Januari 2019, umepungua hadi asilimia 3.0 kutoka asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia mwezi Disemba 2018.
Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephrahim Kwesigabo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema kuwa hali hiyo inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma, kwa mwaka ulioishia mwezi Januari 2019 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Disemba 2018.
Aidha, amesema kuwa kupungua kwa mfumuko wa bei wa taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Januari 2019 kumechangiwa hasa na kupungua kwa bei za vyakula zikilinganishwa na zile zilizoishia mwezi Januari 2018.
“Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Januari 2019 umeendelea kupungua hadi asilimia 0.7 kutoka asilimia 1.0 ilivyokuwa mwezi Disemba 2018,“amesema Kwesigabo.
Kwesigabo amezitaja baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei wa mwezi Januari 2019, ni pamoja na mchele kwa asilimia 3.9, mahindi kwa asilimia 13.9 na unga wa mahindi kwa asilimia 8.9.
Pia amesema kuwa bidhaa zingine ni mtama kwa asilimia 5.1, unga wa muhogo kwa asilimia 6.8, maharage kwa asilimia 4.2, chiroko kwa asilimia10.5, mihongo kwa asilimia 5.6, viazi vitamu kwa asilimia 3.3, magimbi kwa asilimia 18.6 na ndizi za kupika kwa asilimia 13.3.
Hata hivyo, ameongeza kuwa mfumuko wa bei kwa nchi za Afrika Mashariki amesema nchini Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Januari 2019 umepungua hadi asilimia 4.7 kutoka asilimia 5.71 kwa mwaka ulioishia mwezi Disemba 2018, huku Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Januari 2019 umeongezeka hadi asilimia 2.7 kutoka 2.2 kwa mwaka ulioishia mwezi Disemba 2018.