Mfumuko wa bei wa Taifa umeshuka kutoka asilimia 3.6 hadi asilimia 3.4 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti 2019 kutokana na kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za jamii na sensa ya watu toka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ruth Minja wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Dodoma Octoba 8, 2019.

Amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa bei za bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Septemba 2019, zikilinganishwa na bei za mwezi Septemba 2018.

“Kasi ya mabadiliko ya ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba 2019 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2019,” amefafanua Bi. Minja.

Amezitaja baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizopungua bei kwa mwezi Septemba 2019 zikilinganishwa na bei za mwezi Septemba 2018 kuwa ni pamoja na mafuta ya taa kwa asilimia 1.0, Petrol asilimia 3.3, majiko ya gesi asilimia 4.0, Dawa za kuulia wadudu nyumbani asilimia 2.2 na mafuta ya nywele asilimia 1.3.

Aidha Bi. Minja ameongeza kuwa mfumuko wa bei za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba 2019 umeongezeka hadi asilimia 4.0 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti 2019.

“Hali ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki pia imepungua ambapo nchini Kenya kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba 2019 ni asilimia 3.83 kutoka asilimia 5.00, huku Uganda ukipungua kwa asilimia 1.9 kutoka asilimia 2.1 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti 2019,” amesema Bi. Minja.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ni Taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 ikiwa na mamlaka ya kutoa, musimamia na kuratibu upatikanaji wa taarifa za kitakwimu kwa ajili ya matumizi ya Serikali na wadau.

Singida mwenyeji maadhimisho siku ya chakula Duniani
Video: Lupita Nyong'o asimulia alivyonyanyapaliwa kwa weusi wake