Mfumuko wa bei kwa mwaka 2021 uliongezeka kwa wastani wa asillimia 3.7 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.3 kwa mwaka 2020, wakati hadi kufikia Aprili 2022 deni la Serikali lilikuwa Shilingi 69.44 trilioni ikilinganishwa na Shilingi 60.72 trilioni kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 14.4.
Akiwasilisha Mpango wa Maendeleo na hali ya uchumi kwa Taifa kwa mwaka wa fedha 2022/23, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema mfumuko wa bei umeendelea kuwa ndani ya lengo la wigo wa asilimia 3 hadi 5.
“Mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 3.8 Aprili 2022 ikilinganishwa na asilimia 3.3 Aprili 2021 ukichangiwa na sababu zilizo nje ya udhibiti wa Serikali kama kuvurugika kwa mnyororo wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa katika soko la dunia,” amefafanua Waziri Mwigulu
Dkt. Mwigulu ambaye alikuwa akitoa maelezo haya Bungeni jijini Dodoma hii leo Juni 14, 2022, kwa upande wa deni la Taifa amesema kati ya kiasi kilichotajwa deni la nje lilikuwa Shilingi 47.07 trilioni na deni la ndani lilikuwa Shilingi 22.37 trilioni.
“Ongezeko la deni la Serikali lilitokana na kupokelewa kwa mikopo mipya kutoka vyanzo vyenye masharti nafuu na ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo,” ameongeza Waziri huyo.
Hata hivyo, amesema ongezeko la deni lilitokana na kutolewa kwa hatifungani maalumu yenye thamani ya Shilingi 2.18 trilioni, kwa ajili ya deni la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), la michango ya watumishi wa kabla ya mwaka 1999.
“Taarifa ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Novemba 2021, inaonesha deni la Serikali bado ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu kwa kuzingatia ukomo wa viashiria vyote vinavyokubalika Kimataifa,” amesema.