Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba amesema mwaka 2022, mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 4.3 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.7 mwaka 2021.
Nchemba ameyasema hayo hii leo Juni 15, 2023 Bungeni jijini Dodoma, na kuongeza kuwa mfumuko wa bei hadi mwezi Mei, 2023 umebaki kama ilivyokuwa katika kipindi hicho hicho mwaka 2022 ikiwa ni wastani wa asilimia 4.0.
Amesema, “hali hii imesababishwa na kuongezeka kwa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma na kuongezeka kwa upatikanaji wa mazao ya chakula katika baadhi ya maeneo nchini na Nchi jirani kulikosababishwa na upatikanaji wa mvua katika maeneo yanayotegemea mvua.”
Kuhusu miamala ya kutoa fedha benki, Mwigulu amesema imeongezeka kufikia milioni 12.2 ikiwa na thamani ya TZS trilioni 5.4 mwaka 2022 ikilinganishwa na miamala milioni 10.6 yenye thamani ya TZS trilioni 3.5 mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 15.5.