Kinara wa Upinzani nchini Kenya na Kiongozi wa Muungano wa Azimio, Raila Odinga amesema mandamano yao ya kitaifa yataendelea licha ya mazungumzo kuandaliwa, na kwamba atatangaza siku mpya za maandamano baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhan kutamatika.
Hatua hiyo ya Odinga inakuja huku kukiwa na taarifa za uamuzi wa Muungano huo kumuondoa Sabina Chege kama Naibu Kiranja wa wachache bungeni, licha ya pingamizi kutoka kwa chama cha Jubilee ambapo Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula anatazamiwa kutoa uamuzi kuhusu swala hilo.
Hivi karibuni, Kiongozi wa chama cha NARC-Kenya ambacho ni sehemu ya muungano wa Azimio, Martha Karua alisisitiza kuwa ili kudai haki ya wakenya dawa inayofaa ni kutumia njia ya Maandamano huku Baraza kuu la Makanisa nchini Kenya likiunga mkono kauli hiyo.
Viongozi hao wanasema, wanalazimika kufanya maandamano hayo, ili kudai mambo ya msingi kutokana na kupanda kwa gharama za maisha zinazowaumiza wakenya wengi ambapo Rais wa Kenya William Ruto alisema mapatano yafanyike kwa kutumia njia ya mazungumzo Bungeni.