Mfungwa aliyeachiwa huru kwa msamaha wa Rais kutoka gereza la Bukoba Mkoani Kagera avamia stendi kuu ya mabasi na kuwachoma watu visu ambapo amesababisha kifo cha mfungwa mwenzake aliyeachiwa pia kwa msamaha na majeruhi watano na yeye kuuawa na wananchi wenye hasira kali.
Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa polisi Mkoa wa Kagera Revocatus Malimi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, nakusema tukio hilo lilitokea Desemba 13 mwaka huu majira ya saa tatu usiku eneo la stendi kuu ya mabasi Bukoba Manispaa.
Amesema kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa ghafla mtu mmoja asiyefahamika majina yake mwenye umri kati ya miaka (30-35 ) alivamia maeneo ya stendi hiyo na kumchoma kisu tumboni na usoni Godfrey Gobadi ( 35 ) dereva wa bajaji na kumsababishia kifo papo hapo ambaye pia aliachiwa kwa msamaha wa Rais.
Malimi amewataja waliojeruhiwa kuwa ni Michael Bukerebe (26 ) msukuma wa Mwanza fundi magari ambaye amejeruhiwa maeneo ya shingoni na mgongoni, Salum Athuman (35 ) mhaya mkazi wa Omukigusha Bukoba ,amejeruhiwa mbavuni na mkononi.
Wengine ni Jalia Abdi (40 )Mnyiramba na mkazi wa Migera Bukoba wakala wa magari amejeruhiwa mgongoni, Jimmy Mashaeli (45 ) Mhangaza wa Ngara, amejeruhiwa mikono yote miwili na Nasri Abdalah (19), Mdigo fundi Magari mkazi wa Dar-es-salaam .
“Baada ya mtuhumiwa kufanya vitendo hivyo, wananchi wenye hasira kali walimvamia na kuanza kumshambulia na kumuumiza vibaya ambapo askari polisi waliokuwa doria na waliokuwa kituoni waliwahi katika tukio hilo na kufanikiwa kumuokoa mtuhumiwa asiendelee kushambuliwa lakini alifariki wakati akipelekwa hospitali” Ameeleza Kamanda Malimi.
Amesema uchunguzi wa Awali umebaini kwa mujibu wa karatasi “Discharge form” iliyokuwa mfukoni yenye majina ya ( EX –CONV 655/2019 Godfrey Gobadi, iliyokuwa katika mfuko wa nguo zake ni ya marehemu huyo iliyomtoa gerezani kwa msamaha wa Rais.
Kamanda Malimi amesema mtuhumiwa aliyeuawa na wananchi hakuwa na kitambulisho chochote na ametambuliwa kwa asilimia 60 kuwa naye alitoka gereza la Bukoba kwa msahama wa rais na kuwa chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa.
Kwaupande wake kaimu mganga mfawidhi wa hospital ya Rufaa ya Bukoba mkoani Kagera Dk.Mussa Sweya amesema Desemba 13 mwaka huu majira ya saa 3:30 usiku alipokea marehemu wawili wa kiume na majeruhi watano .
Dk.Sweya,amesema katika marehemu wawili aliowapokea mmoja alitambuliwa kwa jina la Gerofrey Kobadi na mwingine hajatambuliwa.
Aidha amefafanua kuwa majeruhi wawili walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka kutokana na kuwa na majeraha madogo na watatu walilazwa kwaajili ya uangalizi wa karibu.
Amewataja waliolazwa kuwa ni Michael Bukerebe (26 ),Salum Athuman (35 ) na Nasri Abdalah (19 ) na kusema kuwa hali zao zinaendelea vizuri.
Amesema Sulum Athuman amefanyiwa upasuaji mkubwa uliochukua muda wa masaa matano na kudai kuwa hali yake inaendelea kuimarika.