Mfungwa aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 25 jela nchini Ufaransa kwa mauaji na ujambazi ametoroshwa kutoka gerezani baada ya watu wenye silaha kutua na helkopita na kisha kuwateka walinzi.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AP, watu hao wenye silaha walikata nondo za mlango na kuingia kwenye chumba cha wafungwa kukutana na wageni, wakati ambapo Redoine Faid alikuwa ametembelewa na kaka yake na kisha wakaondoka naye.
Mwakilishi wa kikosi cha ulinzi wa gereza hilo, Martial Delabroye amekiambia kituo cha runinga cha BFM kuwa watu hao wenye silaha walikuwa wamevalia mavazi ya kuficha sura zao maarufu kama Ninja, pamoja na mavazi mengine maalum ya polisi wa kitengo cha kupambana na ujambazi.
Amesema kuwa chopa iliyokuja na watu hao ilitua eneo pekee ambalo halina vizuizi vya chopa kutua (anti-helicopter netting) na pia waliwasha kifaa cha kutoa moshi mkubwa ili kuhakikisha kamera hazishiki picha kutokana na moshi.
Imeelezwa kuwa watu hao walimteka rubani wa chopa na kumlazimisha kutua katika eneo hilo, wakamchukua Faid na kuondoka naye lakini hawakumdhuru rubani huyo.
Waziri wa Sheria wa Ufaransa ameviambia vyombo vya habari kuwa mfungwa huyo alikuwa amefanya jaribio la kutoroka saa chache zilizopita.
“Walinzi wetu ambao hawakuwa na silaha za moto wamesema kuwa hawakuweza kufanya lolote kuzuia tukio hilo,” alisema.
Alisema baada ya watu hao kukamilisha zaoezi lao, walimuachia huru rubani waliyekuwa wamemteka na kisha kuichoma moto chopa waliyoitumia.
“Chopa ilikutwa kwenye mji wa Garges-les-Gonesse, sehemu ya eneo la jiji la Paris ikiwa imechomwa moto,” amesema.
Aliongeza kuwa waendesha mashtaka wameanza kufanya uchunguzi kuhusu tukio hilo na kwamba wameanza kumhoji kaka yake Faud tangu Jana (Jumapili).
Faid mwenye umri wa miaka 46 alikuwa anatumikia kifungo cha miaka 25 jela kwa kosa la kumuua askari polisi mwaka 2010 katika tukio la ujambazi.
Kumbukumbu za polisi zilionesha kuwa mwishoni mwa miaka ya 1990 aliongoza kundi la majambazi ambalo lilivamia Benki kadhaa. Alikamatwa mwaka 1998 baada ya kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Imeelezwa kuwa aliachiwa mwaka 2009 baada ya kutumikia kifungo cha miaka 10 jela na aliapa kuwa amebadili mienendo ya maisha yake. Aliandika kitabu rasmi kuhusu maisha yake ya kihalifu na kufanya ziara kubwa na maarufu kwenye vyombo vya habari mwaka 2010.
Hata hivyo, mwaka huohuo alituhumiwa kushiriki katika jaribio la wizi wa kutumia silaha za moto uliosababisha purukushani za kufyatuliana risasi kati ya kundi la majambazi na askari polisi, na kusababisha kifo cha askari mmoja mwenye umri wa miaka 26 aliyetajwa kwa jina la Aurelie Fouquet.
Alikamatwa tena mwaka 2011.