Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha vijiji vyote nchini vitakavyo pitiwa na mradi wa Bomba la mafuta la Afrika Mashariki EACOP kupatiwa umeme mapema kabla ya mradi huo kuanza.
Ameyasema alipokuwa akizungumza na Dar24 Media mara baada ya kumalizika kongamano la wadau wa mkoa wa Kagera Manispaa ya Bukoba ambapo ambapo amesema kuwa nishati ya umeme ni nguzo muhimu katika mradi huo, hivyo serikali itahakikisha umeme unasambaa kwa haraka iwezekanavyo katika maeneo yote ambayo mradi huo utapita.
Amesema kuwa kwa upande wa Kagera vijiji vyote ambavyo havijapata umeme tayari vimeshaingia kwenye mpango wa kusambaziwa umeme katika mpango wa leo awamu ya tatu ili kuhakikisha wananchi wanapata matunda ya serikali yao.
Naibu Subira ambaye ni mlezi wa mkoa wa Kagera kwa upande wa Nishati amekiri kuweppo kwa changamoto mbalimbali mkoani Kagera kukiwemo maeneo mengi ambayo utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya pili haukuweza kufika na sasa tayari wizara imeshaanza kuyafanyia kazi.
“Natambua Kagera kuna vijiji ambavyo havina umeme lakini mpango uliopo tupo tunatekeleza Rea awamu ya tatu katika vijiji 134 lakini tupo mbioni kuanza kutekeleza mpango wa Rea awamu ya tatu mzunguko wa tatu ambao utaanza mwezi wa saba, utaratibu uliopo ni kumalizia maeneo yote hayakufikia. Niwape moyo wakazi wa mkoa wa Kagera ambao hawajapata Umeme serikali ya awamu ya tano tutawafikia.” Amesema Mgalu.
Aidha, Mgalu amesema kuwa kama mlezi wa nishati mkoani Kagera ameanza kumsimamia mkandarasi ambaye ni Naclowing Investment ili kuweza vijiji vyote ambavyo havijapata umeme vinapata umeme japo kasi yake haridhishi.
Hata hivyo, ameongeza kuwa gharama za kufungiwa umeme kwa wananchi wote wa vijijini ni shilingi elfu 27,000/= ambapo amesema kuwa baada ya Rea kumaliza mradi na kukabidhiwa Tanesco bei imekuwa ikipanda ambapo aemesama hata kama mradi ukiwa umeshakabithiwa uungaji wa umeme utakuwa bei ile ile.
Amewaomba wakazi wa vijijini hasa wanaopitiwa na mradi wa Rea kuwa na imaani na serikali yao inayoongozwa na Mhe.Rais Magufuli kuwa inawajali wanyonge.