Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma linawashikilia askari wanne wa Jeshi la Akiba la Mgambo kwa tuhuma za kumpiga na kumuua, Liberatus Mkomed (40) mkazi wa kijiji cha Kumhasha.

Akizungumza leo Mei 28, 2021 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, James Manyama amesema tukio hilo limetokea Mei 23, 2021 saa tatu usiku katika kijiji cha Kumhasha  wilayani Kibondo Mkoa wa Kigoma.

Amebainisha kuwa askari hao waliingilia ugomvi wa kifamilia kati ya Mkomed na mkwewe,  Scolastica Bakunda na kuanza kumshushia kipigo mwanaume huyo kwa kutumia fimbo na chuma maeneo mbalimbali mwilini.

Amesema baada ya kufanya tukio hilo, askari hao walikimbia na kwenda kujificha lakini Mei 26, 2021 walikamatwa na polisi.

“Mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi katika hospitali ya Wilaya ya Kibondo Mei 24, 2021 na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi,” amesema Manyama.

Hata hivyo ameeleza kuwa upelelezi wa tukio hilo unaendea na watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya taratibu kukamilika.

Askari afa maji akimkimbiza mtuhumiwa
RPC Dar: Waliotoroka gerezani chanzo kuongezeka kwa uhalifu