Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amepongeza hatua iliyochukuliwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kwa kumsimamisha kazi Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kuvule kufuatia kushindwa kusimamia vyema miongozo ya udhibiti wa magonjwa, katika maeneo ya kutolea huduma za afya.
Waziri Ummy amepongeza hatua hiyo akiwa ziarani Bariadi, Simiyu kukagua ubora wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya ambapo amebainisha kuwa kitendo alichofanya mtumishi wa Kituo cha Afya Kivule kuosha vyombo vya Hospitalini katika hali isiyofaa kuwa hakikubaliki.
“Tumeona mtumishi anaosha vyombo vya Hospitali kwa maji ya baridi na kuanika juani, sijawahi kuona nimefurahi hatua imechukuliwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dar kwa kumsimamisha kazi Mganga Mfawidhi kwa kushindwa kusimamia majukumu yake.” amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy ameongeza kuwa mtumishi huyo amekiuka maadili ya taaluma yake hivyo kuna uzembe kwenye suala ya usimamizi wa miongozo ya afya katika Kituo hicho.