Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amepiga marufuku Wamiliki wa Hospitali Binafsi tabia ya kuwapokea Watumishi wa afya wa Serikali wakati wa muda unaowataka wawe katika vituo vyao vya Serikali.
Dkt. Sichalwe ametoa agizo hilo leo Februari 23, 2022 wakati akiongea na Wajumbe wa Bodi ya ushauri ya hospitali Binafsi, Wataalamu wa afya ngazi ya Mkoa, na Jiji pamoja na Wamiliki wa Hospitali Binafsi Jijini Mwanza.
Amesema, Serikali haina lengo la kumkataza Mtoa huduma yoyote kufanya kazi katika vituo vya kutolea huduma binafsi, bali ni lazima utaratibu ufuatwe ili kuepuka changamoto ya upungufu wa Watoa huduma katika vituo vya Serikali wakati wa muda husika.
“Ni marufuku kumpokea Mtumishi aliyeajiriwa na Serikali, ndani ya muda wa kazi wa Serikali, tukikupata hatutakuwa na huruma, kwasababu tunataka utaratibu ufuatwe Watumishi waje baada ya muda wa Serikali kumalizika.” Amesema Dkt. Sichalwe.
Aidha amewaelekeza Wamiliki hao kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuanzia mgonjwa anapoingia getini, anapopata huduma mpaka anapoondoka ili kuondoa malalamiko yanayoweza kuzuilika, huku akiwasisitiza kuepuka vitendo vya Rushwa na kufanya kazi kwa juhudi na weledi kulingana na taratibu na miongozo ya taaluma zao wakati wa kuwahudumia wananchi ili kuondoa uvunjifu wa haki na malalamiko yanayoweza kuzuilika.
Aidha, amepiga marufuku vitendo vya kutoa dawa zilizopita muda kwa wagonjwa, huku akisisitiza Serikali imeanza kufuatilia hilo na watakaobainika watachukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa watoa huduma wengine.
Pia, Amewaelekeza kufuata Sheria na utaratibu, hasa katika ufunguaji wa Hospitali na Maabara ili kuepuka kuwa na Maabara bubu ambazo nyingi zinatoa huduma kwa viwango duni hivyo kumnyima fursa mwananchi kupata huduma bora za afya.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachunzibwa amemshukuru Mganga Mkuu kwa kutenga muda na kuja kuongea na Wamiliki wa Hospitali Binafsi katika Mkoa wa Mwanza jambo litaloongeza tija katika kuboresha utoaji huduma kwa wananchi