Guinea, Polisi nchini humo wanamshikilia mganga wa kienyeji aliyejulikana kwa jina la N’na Fanta Camara kwa kosa la kutoa tiba ya uongo na kuwalaghai mamia ya wanawake kwa kuwaaminisha kuwa watashika ujauzito.
Mganga huyo aliwarubuni wanawake waliomtaka awatibu tatizo la kukosa uwezo wa kushika ujauzito na kuwapa dawa ya kienyeji iliyosababisha matumbo yao kujaa mithili ya mwanamke mwenye ujauzito.
Camara aliwapa masharti wateja wake akiwaamuru wanawake hao kutohudhuria kwa daktari.
Kutokana na huduma hizo wagonjwa walilipa dola 33 kwa huduma hiyo ambayo kwa nchi hiyo kipato cha kila mwezi kinakadiriwa kuwa dola 48.
Siku ya Jumanne zaidi ya wanawake 200 waliandamana nje ya kituo cha polisi kwenye mji mkuu wa Guinea Conakry ambapo Bi Camara alikuwa akizuiliwa.
Zaidi ya wanawake 700 walio kati ya umri wa miaka 17 na 45 wanaamiwa kuathiriwa na matibabu ya Bi Camara.
Idadi hiyo kubwa inaonesha jinsi Guinea na nchi zingine za Afrika zinawategemea madaktari wa kienyeji.
Bi Camara hata hivyo anasema kuwa hajafanya lolote baya.
“Ninafanya kazi ngumu sana kuwasaidia wanawake kuweza kutimiza ndoto zao lakini mengine yako mikononi mwa Mungu, aliwambia waandishi wa habari mjini Conakry.