Spika wa Bunge Dkt. Tulia Akson amesema mchakato wa kugawanya jimbo la Mbeya mjini haukuanza leo bali ni maono ya aliyekuwa Rais wa awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Magufuli kwa kushirikiana na Wananchi wa Mkoa huo.
Dkt. Tulia ameyasema hayo wakati akifanya mahojiano na vyombo vya Habari jijini Dodoma nakuongeza kuwa hata maneno yanayosemwa kuwa yeye ndiye anataka jimbo hilo ligawanywe pia ni ya kweli yalilenga kuwahudumia wananchi kwa ukaribu.
Amesema, “lile jambo si jambo jipya maombi ya kugawana jimbo la Mbeya hayajatokana na mimi ni maombi ya Wananchi na yalipelekwa kwa aliyekuwa rais wa kipindi hicho Mheshimiwa Magufuli alisema mkichagua CCM kikao cha kwanza cha baraza wajadili mgawanyo wa jimbo.”
Aidha, Dkt. Tulia ameongeza kuwa tayari baraza lilishaanza mchakato kuhusu jambo hilo na kwamba maneno kuwa Spika anataka jimbo hilo ligawanywe yana ukweli kwani ndiyo maendeleo kwani upo uwezekano wa kupata Halmashauri mbili.