Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema Serikali itahakikisha inaweka mgawanyo sawa wa rasilimali za elimu nchi nzima ili kuwezesha watoto wote wa Kitanzania kupata elimu na mazingira bora ya ujifunzaji.
Akizungumza katika uzinduzi wa Mradi wa TEHAMA kwa Shule za Sekondari za Serikali uliofanyika katika Shule ya Sekondari Mawenzi Mjini Moshi Waziri huyo amesema kuwa ni lazima watoto wote wa Kitanzania wapate fursa sawa kwenye elimu bila kujali eneo analotoka.
“Mgawanyo wa fursa za elimu nchi nzima ni lazima uwe sawa na wa haki ili mtoto asije kukosa fursa nzuri kwa sababu amezaliwa katika Wilaya fulani na mwingine wa Wilaya nyingine anapata fursa nzuri zaidi wakati watoto wote hawa ni Watanzania,” amesema Prof. Mkenda.
Profesa Mkenda amesisitiza kuwa Serikali inataka kuona TEHAMA inatumika katika kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu pamoja na kuimarisha ubora wa mafunzo.