Kampuni ya Uchimbaji Mkubwa wa Madini ya Dhahabu wa Barrick kupitia mgodi wake wa Barrick North Mara umepigwa faini ya shilingi bilioni moja baada ya kutokea uzembe uliopelekea bomba la maji taka kupasuka
na kutiririkia kwenye vyanzo vya maji na makazi ya watu.
Akizungumza katika tukio hilo, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema Mgodi wa North Mara unaomilikiwa na Kampuni ya Barrick kwa asilimia 84% na Serikali kwa asilimia 16% unapaswa kuwa mfano bora kwa kufuata na kusimamia Sheria, Taratibu na Kanuni zilizowekwa na serikali.
“Haiwezekani Bomba la maji taka lipasuke saa tatu asubuhi halafu uongozi upate taarifa saa sita mchana na isitoshe kuna walinzi wanaozunguka maeneo hayo, huu ni uzembe wa hali ya juu, sisi tunataka usalama wa watu wetu,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko amembadilishia majukumu Afisa Migodi Mkazi wa Mgodi wa North Mara baada ya kushindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo katika eneo alilopangiwa.
“Kutokana na uzembe huu uliofanyika hapa mgodini naanza na Afisa wangu namuondoa hapa ataenda kupewa majukumu mengine, siwezi kukubali uzembe huu uendelee,” amesema Dkt. Biteko.
Sambamba na hayo, Waziri Biteko ameitaka Kampuni ya Barrick kuhakikisha inachangia katika kuleta maendeleo kwa jamii (CSR) ili wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka Migodi yaweze kunufaika na uwepo wa mgodi huo katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Samuel Gwamaka amesema, Kifungu cha 187 cha Sheria ya Mazingira kinampa mamlaka ya kuipiga faini yenye makosa ya kuvujisha maji taka kuanzia milioni 50 mpaka bilioni 10.
“Kampuni hii ya Barrick tumeipiga faini ya bilioni moja ili iwe mfano kwa wengine, hivyo itambuliwe hilo ni kosa na sisi kama NEMC tutaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha makosa kama haya hayajitokezi,” amesema Dkt. Gwamaka.
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesema bomba hilo lililopasuka linatoa maji katika bwawa linalokusanya maji kutoka kwenye miamba ya mashimo ya dhahabu kwenye mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara na si kwenye bwawa la sumu kama ilivyodhaniwa awali.
Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa, Jerome Kayombo amesema kuna bwawa linalokusanya maji yanayotiririka kwa ajili ya kuhifadhiwa kabla ya kusafirishwa kwa ajili ya kutibiwa na kutumika kwa matumizi ya kawaida.
” Lipo bwawa maalum linalokusanya maji kutoka kwenye miamba ambayo kwa asili yana tindikali kwahiyo yakishajaa kwenye bwawa yanasafirishwa kwenye mfumo kwa ajili ya kutibiwa ili kuingia kwenye mfumo wa matumizi ya kawaida,” amesema.
Amesema kuwa mara baada ya tukio hilo kutokea, juzi wataalam kutoka NEMC walifika katika eneo hilo na tayari wamechukua sampuli za maji kutoka katika maeneo tofauti ikiwemo kwenye mto Tigite ili kupima ubora wa maji hayo.
Naye Meneja wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Ziwa, Musa Kazimila amesema vipimo vya awali vinaonyesha maji katika eneo hilo ni salama, ingawa uchunguzi wa kina unaendelea na majibu yanatarajiwa kutoka Jumatano Aprili 27, 2022.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Ally Happy amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anataka kuona fedha zinatolewa kwa ajili ya miradi inawanufaisha wananchi ambapo ameitaka kampuni ya Barrick kutoa michango yake kwa jamii (CSR) ili kusogeza maendeleo kwa jamii.
Pia, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Mwita Waitara amempongeza Dkt. Biteko kwa kufika eneo la tukio, akisema hiyo inaonyesha ni kiasi gani anajali na anathamini utu wa watu.