Waziri wa Madini, Doto Biteko ameuagiza uongozi wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya Dhahabu MMG GOLD LIMITED unaomilikiwa kwa ubia kati ya Kampuni ya MMG na Polygon kulipa deni la kiasi cha shilingi milioni 36 zinazodaiwa na kijiji kwa mujibu wa mkataba wa uwekezaji.
Waziri Biteko ametoa agizo hilo wa ziara ya kukagua shughuli za uchimbaji katika mgodi wa MMG GOLD LTD katika kijiji cha Seka kata ya Nyamlandililila wilaya ya Musoma Vijijini , Mkoani Mara.
Akizungumza na Mkurugenzi wa mgodi huo Yury Chernomorchenko, Waziri Biteko ametoa miezi miwili deni hilo liwe limelipwa na kampuni hiyo.
Amesema kuwa, kampuni hiyo ilikuwa inadaiwa zaidi ya shilingi milioni 60 toka mwaka 2018 na Serikali ya kijiji kama ushuru, deni lililoachwa na menejimenti iliyopita ya MMG ambapo walilipa fedha kiasi na hadi sasa deni linalodaiwa ni shilingi milioni 36 na kijiji kwa mujibu wa mkataba wa uwekezaji.
“Niwaombe Serikali za mitaa, Vijiji na Halmashauri, makubaliano yoyote wanayoingia na migodi ili yaweze kuwa na nguvu ya Kisheria kwa msimamizi wa migodi ni lazima wayasajili makubaliano hayo kwenye ofisi ya madini.” amesema Biteko