Baada ya mgogoro wa makazi wa Magomeni Kota uliodumu kwa kipindi kirefu  Serikali umeumaliza ambapo  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amesema  Rais John Pombe Magufuli amefuta hati na mikataba yote inayohusiana na ardhi ya yaliyokuwa makazi ya Magomeni Kota, Dar es Salaam.

Wakati akiongea na Kamati ya Mgogoro wa Makazi ya Magomeni Kota mbele ya waandishi wa habari Mh. Lukuvi amesema rais ameondoa umiliki wa eneo hilo toka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kumilikisha Serikali Kuu ambayo ndiyo itakayosimamia ujenzi wa nyumba 644 ambazo zitauzwa kwa bei nafuu kwa waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota.

“Tutajenga nyumba 644 na kuwauzia kwa bei ya jengo na siyo ya ardhi ili kuwapeni unafuu katika kununua,”alisema Lukuvi huku akishangiliwa na baadhi ya wakazi wa Magomeni.

Aidha  amesema kuwa anampongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kumaliza mgogoro huu ambao umedumu kwa muda mrefu na kuongeza kuwa ameagiza timu ya wataalamu wa Wizara kupima na kuchora michoro kwa ajili ya ujenzi.

Lukuvi amesema katika eneo hilo zitajengwa nyumba ambazo kila moja itakuwa na vyumba vitatu ili kukidhi mahitaji ya kifamilia kwani watu hao wamekaa kwa takribani miaka 50 hadi wameshapata wajukuu na kuongeza kuwa kila mmiliki wa nyumba hiyo atapewa hati yake hata kama nyumba hiyo itakuwa kwenye ghorofa.

Pamoja na hayo Mh Lukuvi ametoa agizo la Rais kuwa sehemu zingine kama Magomeni Kota katika mikoa ishirini ya Tanzania Bara nazo zitakuwa katika mfumo huokama huo wa Magomeni huku akisisitiza wazee ambao wanakaa kwenye nyumba kama wasiondolewe kwani walikuwa watumishi wa umma hivyo wasisumbuliwe.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mgogoro wa Makazi Magomeni Kota, George Abel ameshukuru Rais Magufuli na Wazir Lukuvi kwa kutatua mgogoro huo ambao anadai umewasumbua sana na kuahidi kutoa ushirikiano kwa Serikali pindi suala la ujenzi litakapokuwa linaendelea ili kuhakikisha ujenzi unaenda haraka.

 

Uamuzi wa kurudisha eneo hilo kwenye Serikali Kuu umetolewa na Rais Magufuli tarehe 10/7/ 2016.

Video: Pestana CR7 Hotel ya Cristiano Ronaldo
Video: Ugonjwa wa Sumu Kuvu watajwa kuwa changamoto kubwa