Matukio ya ajali kwa wagombea wanaoendelea na mchakato wa kampeni katika uchaguzi mkuu yanayendelea kuwakumba baadhi ya wagombea ambapo jana mgombea ubunge wa jimbo Kwela Kwa tiketi ya Chadema, Daniel Naftari Ngogo alinusurika baada ya gari lake kupata ajali.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Ferdinand Rwegasira alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya gari alilokuwemo mgombea huyo pamoja na watu watatu kushindwa kupanda mlima Ilemba na kuanza kurudi nyuma kabla ya kuanguka.

Mgombea ubunge wa Chadema, Jimbo la Kwela, Naftari Daniel Ngogo (Kulia), akikabidhiwa fomu na Katibu wa Chadema wilaya ya Sumbawanga mjini, Pius Nguvumali

Mgombea ubunge wa Chadema, Jimbo la Kwela, Naftari Daniel Ngogo (Kulia), akikabidhiwa fomu na Katibu wa Chadema wilaya ya Sumbawanga mjini, Pius Nguvumali

Kamanda Rwegasira alisema kuwa watu watatu waliokuwa kwenye gari hilo walipata majeraha na wanaendelea kupata matibabu katika hospitali ya Ilemba lakini mgombea ubunge huyo hakupata majeraha yoyote.

“Ni kweli mgombea wa ubunge kwa tiketi ya Chadema aitwae Daniel Naftari alikuwa miongoni mwa abiria waliokuwa katika gari hilo lakini kwa bahati nzuri yeye hakupata majeraha,”alisema.

Katikati ya mwezi Septemba, Chadema walipata pigo baada ya mgombea ubunge wa jimbo la Lushoto, Mohamed Mtoi kufariki katika ajali ya gari wakati alipokuwa akitoka kwenye mkutano wa kampeni mkoani Tanga.

 

TFF Yasaini Kandarasi Ya Miaka Mitatu Na Star TV
Ademi Alitumia Dawa Za Kusisimua Misuli