Mtoto mwenye umri wa miaka mitano anapatiwa matibabu nchini Uganda baada ya kubainika kuwa ana ugonjwa wa Ebola.
Waziri wa Afya, Dkt. Jane Ruth Aceng amethibitisha taarifa hizo na kueleza kuwa mtoto huyo aliingia nchini humo akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) akiwa na familia yake.
“Tunathibitisha kuwa anayetibiwa kwa ugonjwa wa Ebola ni mtoto mwenye umri wa miaka mitano, raia wa DRC aliyeingia nchini Juni 9, 2019 kupitia mpaka wa Bwera akiwa na familia yake,” alisema Dkt. Aceng alipozungumza na waandishi wa habari jana.
Aliongeza kuwa Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO) wametuma timu ya wataalam katika Wilaya ya Kasese kwa ajili ya kumfuatilia mgonjwa huyo pamoja na watu waliokuwa naye.
Dkt. Aceng amesema kuwa watu wanane ikiwa ni pamoja na wazazi wa kijana huyo wamepelekwa katika eneo maalum lililotengwa ili wapatiwe matibabu.
Aliongeza kuwa maafisa wa Wizara ya Afya wa DRC wameanza kuwatafuta wanafamilia wa mtoto huyo ambao hawakuvuka mpaka ili waweze kuwafanyia uchunguzi wa kitabibu.
Uganda imekuwa katika tahadhari ya hali ya juu dhidi ya Ebola hasa kutokana na eneo la Mashariki mwa DRC lililoripotiwa kuwa na wagonjwa zaidi ya 2,000 wa Ebola.