Misri imethibitisha kutokea kifo cha kwanza kilichotokana na Virusi vya Corona baada ya raia wa Ujerumani kupoteza maisha, Jumapili, Machi 8, 2020.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya nchini humo, raia huyo wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 60 alionesha dalili ikiwa ni pamoja na kuwa na homa kali alipofika Hurghana akitokea jijini Luxor.
Mshauri wa Waziri wa Afya, Dkt. Khaled Mujahid ameeleza kuwa mgonjwa huyo alilazwa katika hospitali kuu ya Hurghada tangu Ijumaa akipatiwa matibabu.
Jumamosi, vipimo vilionesha kuwa ana virusi vya Corona na kuanzia wakati huo alihamishiwa kwenye chumba maalum hadi alipopoteza maisha saa chache baadaye.
Virusi hivyo ambavyo kwa mara ya kwanza viliripotiwa nchini China, Desemba mwaka jana na kupewa jina la COVD-19, vimeshasambaa katika nchi takribani 95 duniani.
Takribani watu 109,400 wameripotiwa kuwa na Virusi vya Corona na watu 3,500 wamepoteza maisha kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).