Kocha Mkuu wa Simba Queens, Juma Mgunda amesema michuano ya Ngao ya Jamii imekuwa kipimo kizuri kujua timu yake ipoje kuelekea mwanzo wa Ligi Kuu ya Wanawake inayotarajiwa kuanza Desemba 20, mwaka huu.
Simba Queens imekuwa mabingwa wa kihistoria baada ya kutwaa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga JKT Queens kwa penalti 5-4 baada ya sare ya bila kufungana dakika 90 za mchezo huo.
Kabla ya kuweka wazi matarajio yake kwa msimu huu 2023/24, Mgunda amelipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuandaa mashindano hayo kwani yamempa kipimo kizuri kwa timu yake.
“Nashukuru kwa kutwaa ubingwa huu, kwani mashindano yalikuwa magumu na yametufanya tujue tunajiandaaje na ligi, maana JKT Queens ndio washindani wetu hivyo tunajua tunajiandaa vipi,” amesema mshambuliaji huyo wa zamani wa Coastal Union.
Naye Kocha wa JKT Queens, Ester Chabruma kwa upande wake amesema wanakwenda kujiandaa na ligi kutetea ubingwa wao walioutwaa msimu uliopita.
“Mchezo ulikuwa mgumu na matokeo ndio hayo, sasa hivi tunaangalia mbele tukianza na kufanyia kazi makosa yaliyotufanya tukose ubingwa” amesema Chabruma.
Wachezaji wa Simba Queens, Vivian Corazone alichaguliwa mchezaji bora wa mashindano na mlinda mlango Carolyene Rufa akiibuka golikipa bora huku Stumai Abdallah wa JKT Queens akiibuka mhezaji bora wa mashindano na mchezaji bora wa mchezo wa fainali.