Wakati sakata la kampuni ya GSM la kudhamini/kufadhili klabu zaidi ya moja katika Ligi Kuu, likifika kwenye mamlaka za serikali, Mwenyekiti wa Bodi ya ligi ‘TPLB’ Steven Mnguto ametoa maoni yake.
Mguto ambaye ni mwenyekiti wa klabu ya Coastal Union inayodhaminiwa na Kampuni ya GSM amesema sio kosa kwa kampuni moja kudhamini zaidi ya klabu moja katika Ligi Kuu.
Amesema kinachoendelea mitandaoni ni kuwakatisha tamaa wenye kampuni ambao wapo tayari kudhamini/kufadhili klabu za soka ambazo zimekua zikilia ukata kila kukicha.
Mguto amesema: “Kuhusisha upangaji wa matokeo na udhamini ni kujaribu kudidimiza juhudi za vilabu kukuza uchumi wao kwa njia halali”
“Udhamini biashara kama biashara nyingine zinazofanyika. Hizi timu zetu ndogo zinapitia changamoto nyingi sana”
“Kudhamini ni jambo moja, kupanga matokeo ni jambo lingine. Tuepeke sana kujenga ajenda mbaya pasi na sababu zenye mashiko.”
Tayari Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo Innocent Bashungwa amesema sakata hilo litapatiwa ufumbuzi kwa kuzingatia misingi ya kanuni za uendeahaji soka nchini chini ya TFF na Baraza la Michezo Taifa ‘BMT’.