Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Jacob Nyangusi amekamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za rushwa ya ngono.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Takukuru mkoa wa Dodoma, mwalimu huyo alinasa kwenye mtego na kukutwa akiwa na mwanafunzi wa kike wa mwaka wa kwanza katika chumba chake cha kulala, nyumbani kwake.

Mkuu wa Takukuru mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo amesema kuwa mwalimu huyo aliyekutwa nyumbani kwake na mwanafunzi huyo eneo la Nyumba Mia Tatu, Nzuguni jijini Dodoma aliwekewa mtego baada ya mwanafunzi huyo kudai kuwa alimuomba rushwa ya ngono ili amsaidie kutorudia mtihani wa somo alilokuwa anafundisha.

“Mtuhumiwa alikamatwa baada ya kunasa kwenye mtego wa Takukuru baada ya kumchukua mwanafunzi kwa lengo la kufanya naye mapenzi nyumbani kwake ili amsaidie asirudie mtihani wa somo analofundisha,” alisema mkuu huyo wa Takukuru – Dodoma.

Aliongeza kuwa taasisi hiyo imekuwa ikipokea malalamiko mengi ya wanafunzi kuhusu walimu wanaowashawishi ili wawapate kimapenzi kwa kuwahadaa kuwa watawasaidia katika masomo yao.

“Kuna baadhi ya wahadhiri wasio waaminifu wamefikia hatua ya kuwafelisha wanafunzi ili wawatengenezee mazingira ya kufanya makosa hayo,” aliongeza.

Alisema kuwa suala hilo linasubiri kibali cha Mwendesha Mashtaka wa Serikali ili mtuhumiwa aweze kufikishwa mahakamani.

Taasisi hiyo imeeleza kuwa inaendelea kufanyia uchunguzi malalamiko yaliyowasilishwa na wahanga wa rushwa ya ngono.

Majaji watumbuliwa kwa rushwa
Jiji la Dar kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON