Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu). Jenista Mhagama amezindua mfumo mpya wa Kielektroniki wa Kufuatilia Utekelezaji wa Ahadi, Ilani ya Chama Tawala na Maagizo ya Viongozi Wakuu ulioanzishwa kwa lengo la kusaidia upatikanaji na utoaji wa taarifa za utekelezaji kupitia mfumo wa kisasa (kidigitali).
Ameyasema hayo mjini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, amesema kuwa mfumo huo kuwa umejikita katika kusaidia Viongozi Wakuu kupata Taarifa za utekelezaji wa Maagizo yao na yale yaliyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala.
“Mfumo huu utasaidia sana katika kufuatilia shughuli za Serikali ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa maazigo yote na ahadi zilizotolewa ili kuona utekelezaji wake kwa urahisi tofauti na ilivyokuwa awali” amesema Waziri Mhagama.
Amesema kuwa, kuanzishwa kwa mfumo huo ni moja ya sehemu ya kuondoa changamoto kadhaa ikiwa ni kuongeza ufanisi maeneo ya kazi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Hamisi Mwinyimvua amebainisha kuwa mfumo huo umepitia hatua zote muhimu ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha Mawaziri wote, Makatibu Wakuu wote, Wasaidizi wa Rais Dkt. Jonh Magufuli na Watendaji wa Serikali.
Hata hivyo, Mhagama ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao kwa kuona umuhimu wa kuwepo kwa mfumo huo na kutoa rai kwa Watendaji wote wa Serikali kuutendea haki kwa kufanya kazi bila uzembe wowote.