Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Antony Sanga amewaagiza Wakala wa Usambazaji Maji Mijini na Vijijini (RUWASA), kukamilisha mradi wa maji ndani ya siku 60 katika jimbo la Makete Mkoa wa Njombe.
Ametoa agizo hilo wakati akiwa katika ziara Jimbo la Makete ambapo waliongozana na Mbunge wa Jimbo hilo, Festo Sanga na kutembelea mlima wa Kisajanilo kufuatilia chanzo cha mradi wa maji ya Ilolo-Bulongwa ili mradi huo uanze kufanya kazi mara moja.
Wakiwa katika eneo hilo Sanga amesema amepata changamoto hizo za maji katika jimbo hilo kutoka kwa Mbunge ambapo amesema kuwa amekuwa akimkumbusha kila wakati ili mradi huo uweze kuwasaidia wananchi kupata huduma ya maji safi na salama.
“Rais anawapongeza kwa jitihada za kuibua miradi na kutumia nguvu zenu kuianzisha…mmeanzisha mradi huu miaka miwili imepita, Mbunge amenisumbua sana na nimefanya naye vikao zaidi ya mara tatu juu ya hali ya maji makete na jana nilikuwa Shinyanga lakini nimetembea usiku kucha kufika Makete ili tushughulikie changamoto za maji.” amesema Sanga.
“Serikali ni sikivu na ninawaagiza RUWASA ndani ya siku 60 mradi huu ukamilike, Jumanne tutaleta milioni 100 za kuanzia.” amesisitiza Mhandisi Sanga.