Mahakama nchini Misri imemhukumu tajiri mmoja na mfanyabiashara mkubwa aliyekuwa na uhusiano wa karibu na serikali kifungo cha miaka mitatu jela kwa kuhusika katika biashara haramu ya kusafirisha binadamu na shambulio la aibu kwa wasichana wenye umri mdogo katika kituo cha watoto yatima alichoanzisha.
Mohamed El-Amin – ambaye alikuwa anamiliki vyombo vingi vya habari vyenye ushawishi mkubwa, alikamatwa mapema mwaka huu baada ya madai ya unyanyasaji wa kingono katika kituo hicho cha watoto yatima kuwekwa hadharani na shirika la misaada ya kibinadamu liitwalo Missing Children.
Mwendesha mashtaka wa serikali amesema kuwa alitumia mamlaka yake na mazingira magumu ya wasichana hao.
Mamlaka ilifunga kituo hicho cha watoto yatima mwishoni mwa mwaka jana baada ya madai dhidi ya el-Amin kuibuka.
Alikamatwa Januari na tangu wakati huo amekuwa gerezani, El-Amin anaweza kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.