Wananchi Wilayani Ludewa Mkoani Njombe, leo tarehe 15 Oktoba 2019, wameungana na Familia pamoja na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Ludewa mjini, kuadhimisha misa ya Kumbukumbu ya miaka minne tangu Kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ludewa Hayati Deo Filikunjombe kilichotokea Oktoba 15, 2015.

Misa ya Kumbukumbu ya Kuwaombea Hayati Deo Filikunjombe na marafiki zake Egd Nkwera na Kasablanca Haule waliofariki Pamoja kwenye ajali ya ndege iliyotokea katika hifadhi ya wanyama Selous mkoani Morogoro, imeongozwa Leo, na Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Ludewa Mjini, Cathberth Mlowe.

Akiendesha misa hiyo ya kumbukumbu, Padre Cathbert Mlowe ametoa wito kwa waumini wa Dini ya kikristo na Dini nyingine nchini kuishi maisha ya kumpendeza Mwenyezi Mungu, kwa kuwa na upendo kwa Jamii, pamoja na kutenda matendo mema ambayo baada ya kifo jamii itawakumbuka kwa matendo hayo.

“Leo tunamkumbuka Deo Filikunjombe na wengine waliotangulia mbele za haki, Deo aliishi vyema na Jamii ndiyo maana kila wakati watu wanamlilia, Tujiulize wewe na mimi Baada ya kifo Jamii itatukumbuka kwa lipi? Ni lazima tuwe wacha Mungu” Amesema Padre Cathbert Mlowe.

Dkt, Philip Filikunjombe mdogo wake Hayati Deo Filikunjombe akizungumza Kanisani hapo kwa niaba ya familia, amewashukuru wananchi wa Ludewa na maeneo mengine nchini kwa namna walivyofanya kazi na Deo Filikunjombe na kwa kuendelea kujitokeza kushiriki misa ya kumbukumbu ya kifo cha kaka yao mpendwa.

Baadhi ya wananchi walioshiriki Misa hiyo wamesema wanamkumbuka Hayati Deo kwa utendaji wake uliotukuka kwa wananchi ikiwemo kutetea haki zao, na kuboresha huduma za Jamii kama sekta za Afya, Elimu, Umeme Vijijini, sekta ya michezo na miundombinu ya Barabara hasa kipindi cha Masika.

Frank Mseya Diwani wa kata ya Ludende Wilayani Ludewa, amesema alifanya kazi na Deo Filikunjombe hivyo alimfahamu vyema kutokana na utekelezaji wake wa ahadi alizozitoa kwa wananchi pamoja na kuwa jirani na jimbo lake jambo lililomsaidia kutambua matatizo ya Ludewa na kuyashughulikia kwa wakati.

Misa ya kumbukumbu ya Hayati Deo Filikunjombe imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali Wilayani Ludewa akiwemo Mwenyekiti wa CCM, Stanley Kolimba, Katibu wa CCM, Bakari Mfaume, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Mhe, Andrea Tsere na Madiwani wa kata mbalimbali Wilayani hapo.

Hayati Deo Filikunjombe, Egd Nkwera, Casablanka Haule na Rubani wa Ndege hiyo Capt, Silaa walifariki Dunia Oktoba 15 Mwaka 2015 siku chache kabla ya uchaguzi Mkuu kufanyika wakitokea Jijini Dar es Salaam kurejea Wilayani Ludewa, kwenye kampeni wakati Filikunjombe akitetea kiti cha Ubunge.

Pyramids Fc 'kuwaburuza' Yanga CAF
Necta yatangaza Matokeo darasa la Saba, msichana kinara Taifa