Mshambuliaji wa pembeni wa klabu Bingwa Tanzania Bara na Kombe la Shiriksho (ASFC) Simba SC, Shiza Ramadhan Kichuya, huenda akajiunga na Namungo FC kwa mkopo kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu.

Taarifa za ndani kutoka Klabu ya Simba, zimeeleza Kichuya, anatarajiwa kupelekwa Namungo FC kwa mkopo baada ya kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Sababu zinazotajwa kuhusu mpango wa Kichuya kupelekwa kwa mkopo Namungo FC, ni kufuatia klabu hiyo ya mkoani Lindi kuwa na tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa (Kombe la Shirikisho Afrika), hivyo anaweza kucheza na kurudisha kiwango chake.

Kichuya alijiunga na Simba SC kwenye usajili wa dirisha dogo akitokea Klabu ya ENPPI ya Misri, na hajawa na msimu mzuri chini ya Kocha Sven Vandenbroeck.

Kocha wa Namungo, Hitimana Thierry, amesema habari za Kichuya kutarajiwa kujiunga na klabu hiyo, ni kweli amezipata na endapo zitakuwa kweli ana imani kubwa nyota huyo ataisaidia timu yake kutokana na uzoefu mkubwa wa winga huyo kwenye michuano ya kimataifa.

Amesema katika ripoti yake amependekeza kusajili jumla ya wachezaji wanane wa nafasi tofauti ikiwamo anayocheza Kichuya, hivyo kumpata winga huyo, kutamsaidia katika kutekeleza malengo yake.

“Nitakutana na viongozi kukabidhi ripoti ya msimu huu, nimependekeza wachezaji nane kuelekea msimu mpya, wakiwamo mabeki watatu, kiungo wakabaji watatu na washambuliaji wawili kwa ajili ya kuimarisha kikosi chetu kulingana na michuano tutakayoshiriki ili kuhakikisha wanatusaidia kufanya vizuri,” amesema Hitimana na kuongeza:

“Sasa nimepata funzo nahitaji kusajili wachezaji wazuri ili kupata kikosi kipana ambacho kitasaidia timu yetu, ukizingatia msimu huu tutakuwa na mechi nyingi tukianza na Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, lakini kuna mechi za Ligi Kuu pamoja na kimataifa, hivyo tutatakiwa kujenga kikosi imara.”

Kuhusu mustakabali wake ndani ya kikosi hicho, amesema hadi sasa hakuna ofa kutoka timu yoyote iliyohitaji huduma yake zaidi ya Namungo, ambayo wanatarajia kuanza mazungumzo hayo leo baada ya kukabidhi ripoti yake.

“Muda ni mfupi, nimetoa siku 10 kwa ajili ya mapumziko kwa wachezaji ambao wataendelea kutumikia timu hii, juma la kwanza tutakuwa na maandalizi magumu pamoja na kuhakikisha naweka sawa wachezaji wapya na watakaobaki kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wetu wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba,” amesema Hitimana.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Agosti 6, 2020
Tetesi: Aissa Mandi anukia Liverpool

Comments

comments