Kiungo wa Arsenal Calum Chambers yupo katika hatua za mwisho za kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kukamilisha mpango wa usajili wa mkopo wa kujiunga na klabu ya Middlesbrough inayoshgiriki ligi kuu ya soka nchini England (PL) msimu huu.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 21, alijiunga na Arsenal mwezi Julai mwaka 2014 akitokea Southampton kwa ada ya Pauni milioni 16, na tayari ameshacheza michezo 59 akiwa na kikosi cha Arsene Wenger.

Chambers alifunga moja ya mabao matatu ambayo hayakutosha kuikomboa Arsenal na kichapo cha mabao manne kilichotolewa mwanzoni mwa msimu huu dhidi ya Liverpool katika uwanja wa Emirates.

Klabu ya Middlesbrough ambayo imefikia makubaliano na uongozi wa Arsenal ya kumsajili Chambers kwa mkopo, imekua na mwanzo mzuri katika mshike mshike wa ligi kuu ya soka nchini England, baada ya kuambulia ushindi katika mchezo mmoja na kupata sare kwenye michezo miwili.

Kusajiliwa kwa Chambers klabuni hapo huenda kukatoa mchango mkubwa katika safu ya kiungo na ulinzi, hivyo meneja wa Boro Aitor Karanka atakua na chagizo la kumtumia mahala atakapoona inafaa.

Chambers anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Boro, kitakachocheza mchezo ujao wa ligi kuu ya soka nchini England dhidi ya Crystal Palace Septemba 10.

Katika hatua nyingine Chambers atakuwa mchezo wa kumi kusajiliwa na klabu hiyo ya Riverside Stadium katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi.

Majaliwa apokea Sh. Mil. 50 kutoka NNSF
CECAFA Kuanza Kushindanisha Timu Za Wanawake