Aliyekuwa mpiga gitaa maarufu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC, Lokassa Kasia Denis maarufu kama Lokassa ya Mbongou ambaye alifariki miezi sita iliyopita, bado hajazikwa jambo ambalo limezua wasiwasi miongoni mwa mashabiki walio katika Taifa lake na wale wa Ulimwenguni kiujumla.
Lokassa alifariki katika Hospitali ya St. Josephs iliyopo Nashua nchini Marekani Machi 14, 2023 akiwa na umri wa miaka 80 baada ya kuugua kwa muda mrefu na mwili wake kurejeshwa Kinshasa mwezi Aprili, ambapo ulihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Baada ya kuwasili, mwili huo ulipokelewa uwanja wa ndege na wanamuziki wenzake, familia, ndugu, mashabiki na Viongozi wa serikali, huku Maafisa wa Muungano wa Muziki wa Kongo, Blaise Bula na Adios Alemba wakiongoza waombolezaji katika kuupokea mwili wa mwenzao.
Hata hivyo, katika mahojiano ya hivi karibuni na kituo kimoja cha Televisheni, watoto wawili wa Lokassa walitoa wito kwa Serikali ya DRC, kusaidia mipango ya mazishi yake na taarifa kutoka Kinshasa zinasema Wizara ya Utamaduni na Sanaa ingeshiriki kwa kina katika mipango ya mazishi kama ilivyokuwa kwa magwiji wengine wa muziki wa Kongo.
Mwanamuziki Gwiji wa Gitaa la Besi, Godessy Mbemba maarufu kama Lofombo, alisema bado haijafahamika iwapo ni familia yake au Viongozi wa Serikali wanaofanya mipango mazishi, ingawa utaratibu wa kuchelewesha maziko ni kawaida kwa Wakongo kama ilivyokuwa kwa Marehemu Tshala Muana, Madilu Mult System, La General Defao na wengine.