Maafisa wawili wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wamesimamishwa kazi baada ya kubainika kuruhusu uingizwaji wa mifuko mbadala isiyokidhi vigezo katika mpaka wa Tanzania na Kenya.
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Yusuph Ngenya amewataja watumishi aliowasimamisha kazi kuwa ni Emmanuel Kiwango na Jenifa Jackson, ambao amesema waliruhusu uingizwaji wa mifuko hiyo wakijua haikidhi viwango.
“Nimeamua kuwasimamisha kazi watumishi hawa wakati uchunguzi ukiendelea,” alisema Dkt. Ngenya. “Inawezekana kama wameweza kupitisha mifuko hiyo wakati wakijua kuwa haikidhi viwango, ni jambo ambalo wamezoea kufanya hata kwa bidhaa nyingine,” aliongeza.
Dkt. Ngenya alisema kuwa watumishi hao walifanya kosa hilo Agosti 5, 2019 katika mpaka wa Sirari.
Kumekuwa na malalamiko katika baadhi ya maeneo kuhusu kuwepo kwa mifuko mbadala isiyokidhi vigezo, ambayo hutatuka baada ya kuwekewa mzigo kidogo kulingana na uwezo unaokisiwa.
Serikali iliruhusu uingizwaji wa mifuko mbadala baada ya kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki nchini katikati ya mwaka huu.