Faisary Ahmed – Kagera.

Wataalam wa ngazi za vituo vya Afya, wametakiwa kuimarisha mfumo wa kuchakata takwimu na kufanya makadirio sahihi ya bidhaa za afya zinazopatikana Bohari ya Dawa nchini – MSD, ili kuepuka kupewa huduma tofauti na makisio.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Bohari ya Dawa – MSD, Kanda ya Kagera, Kalendero Masatu katika kikao cha wadau wa MDS Kanda ya Kagera kilichofanyika Manispaa ya Bukoba ambapo amebainisha kuwa hali ya upatikanaji dawa imeongezeka kutoka 55% hadi 65% kutoka Julai 2022 hadi Juni 30, 2023.

Amesema, “ni mategemeo yetu kama kanda na menejimenti kwamba mwaka huu tunaouanza upatikanaji wa dawa utakuwa ni mkubwa na tunakadiria tutafika 70% mpaka 80% ndani ya MSD lakini upatikanaji wa dawa kwenye vituo vyetu ni makubwa zaidi ya hapo.”

“Changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza ni uchakataji wa taarifa ili mteja apate anachokihitaji, kuna mapungufu machache bado yapo kwenye maeneo yetu ambapo wengine wanaagiza dawa pengine kiasi kikubwa au kidogo zaidi ya kile alicho otea kwahiyo kupitia kikao hiki tumewataka watendaji wakawakumbushe na kuwapa elimu ili kuondokana na changamoto hii,” amesema Masatu.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Omary Sukari amewasisitiza ngazi ya vituo kufanya makadirio ya dawa vizuri ili kukidhi mahitaji ya watumiaji na kusema, “tuimarishe mfumo wa takwimu ili mtaalamu wa kituo aweze kujua kile anachokiona anapotunzia dawa ni sahihi kwa kilichopo kwenye mfumo na atumie takwimu za wagonjwa kwenye kituo chake ili kuhakikisha anaagiza dawa au vifaa kwa mujibu wa matumizi ya hizo bidhaa za afya.”

Kwa upande wake Meneja wa huduma kwa Wateja na Miradi kutoka Makao Makuu ya MSD, Dkt. Pamella Sawa amesema lengo lao ni kuhakikisha wateja wanapata huduma bora kuanzia anapoagiza dawa na vifaa tiba wavipate kwa wakati.

Kupitia kikao hicho kilichowashirikisha Waganga wakuu, wafamasia wa wilaya na Wataalam wa Maabara kutoka Mikoa ya Geita na Kagera, wameahidi kupitia elimu waliyoipata kuboresha huduma ili kupunguza malalamiko ya wananchi.

Thomas Tuchel uso kwa macho na Harry Kane
Banda, Onyango waivuruga Simba SC