Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema kuna uhitaji wa mifumo thabiti itakayosaidia utatuzi wa migogoro baina ya watu na makundi mbali mbali kwa lengo la kurejesha uwajibikaji kwa viongozi nchini bado ni tatizo na hivyo.
Othman ameyasema hayo Mtoni mjini Zanzibar, wakati akikifunga mradi wa amani yetu, mshikamano
wetu uliosimamiwa na kuendeshwa na Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar – ZAFELA, na shirika Konrad Adenauer Stiffting (KAS) kutoka ujerumani.
Amesema, hatua hiyo ni kwa mujibu wa hulka za kibinaadamu ambapo sio jambo rahisi kuishi bila kuwepo migogoro ya aina mbali mbali kwa kuwa huwepo tafauti miongoni mwa binaadamu zinazotokana na hisia, fikra na mapenzi na kwamba tafauti hizo ndio huzaa migogoro.
Aidha, Othman ameongeza kuwa “ni wajibu wa wanaadamu inapotokea migogoro mbali mbali kujitahidi kuitatua kwa njia za kistaarabu kama vile mijadala na majadiliano hasa inapoendeshwa na kusimamiwa vyema jambo linalosaidia kuepusha vurugu lisitokee.”
Hata hivyo, amesema iwapo nchi inataka kutoka katika migogoro na kujenga amani ya kweli, utulivu na mshikamano endelevu, ni lazima kutanabahi na kupigania uwepo wa maegeuzi na mfumo utakaorudisha uwajibikaji kwa kujenga taasisi imara za umma.