Wadau wa Haki za Binadamu Zanzibar wameshauri kuimarishwa kwa mifumo ya utawala bora wa sheria, ili kuhakikisha uwajibikaji na upatikanaji wa haki kwa wote unafikiwa katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.
Maoni hayo yametolewa katika mdahalo ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar – TAMWA ZNZ, kwa kushirikiana na Shirika la Foundation for Civil Society – FCS, kuhusu utawala bora wa sheria, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na Watoto.
“Ukifuatilia hizi sheria tulizonazo utagundua hakuna hata sheria moja iliyoandikwa kwa lugha za nukta ili kuwawezesha watu wenye ulemavu nao kuzisoma na kuzielewa kwa urahisi hizi sheria, kuna haja sasa ya sheria huzi zitafsiriwe kwa lugha ya nukta, huu ndio utawala bora wa sheria wenyewe kwa upatikanaji wa haki sawa kwa wote,” alisema mmoja wa washiriki Said Suleiman Ali.
Akifungua mdahalo huo, Mwenyekiti wa TAMWA ZNZ, Asha Abdi watumia siku hizo 16 kuhimiza jamii kuwekeza katika utawala wa sheria ili kupata haki bila kujali hali zao, ikiwemo kukabiliana na changamoto zinazopelekea uvunjifu wa haki za binaadamu.
Kuhusu Utawala wa Sheria na upatikanaji wa sheria bora alisisitiza umuhimu wa sheria zilizopo kuhafamika na watu wote ili kuondoa mianya ya ukandamizaji wa haki za wengine, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar, Dkt. Salum Suleiman alisema Wananchi wakiwa na ufahamu wa sheria za masuala mbalimbali, itawasaidia kuepuka makosa mbalimbali hasa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Moja ya misingi ya utawala wa sheria ni lazima sheria zinazotumika zifahamike na watu wote, na ili hilo liweze kufikiwa ni lazima kuwe na mfumo imara wa kuhakikisha upatikanaji wake unakuwa rahisi,” alisema Dkt. Suleiman.
Aidha, Nabir Mohamed Mussa kutoka ZAFAYCO, alisisitiza wadau hasa serikali kubadili mwelekeo wa kukabiliana na tatizo la ukatili kwa kutazama zaidi chanzo cha watu hasa vijana kujiingiza katika vitendo vya udhalilishaji kuliko kupambana na utoaji wa hukumu kali jambo ambalo wakati mwingine halisaidii kutatua tatizo.
Amesema, “ukifuatilia utagundua kesi za udhalilishaji zimeshindwa kumalizika kutokana na serikali imewekeza nguvu zaidi katika kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa badala ya kuwekeza katika kutibu mizizi ya chanzo cha vitendo hivyo, watu wanafungwa lakini ukikaa chini na kuangalia utagundua tatizo sio kuwafunga tatizo lipo huku kwenye jamii yenyewe kuanzia malezi, tunahitaji kurekebisha kuanzia huku.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Pamoja Youth Initiative, Rashid Mwinyi alisema upatikanaji wa sheria zinazotungwa ni changamoto kwa wananchi wa kawaida kutokana na kukosekana kwa mfumo maalum unaowezesha watu wanapohitaji kusoma sheria kuzipata kwa urahisi jambo linalopelekea wengi kushindwa kuzijua sheria zinazowahusu.
Awali, Tatu Abdalla Msellem, Mratibu wa Taasisi ya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE), alishauri umuhimu wa kupatikana sheria moja ya kusimamia kesi za udhalilishaji ili kuondoa changangamoto zinazokwaza upatikanaji wa haki wa waathirika wa vitendo hivyo.
Awali akichangia kwenye mdahalo huo, Sarah Omar, Hakimu wa Mahkama ya Mkoa, alisema mahakama hutekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria zilizotungwa bila kujali matakwa ya mtu au kundi fulani.
Mdahalo huo, umeandaliwa na chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar – TAMWA ZNZ, kwa kushirikiana na Shirika la Foundation For Civil Society – FCS,) ukiwaleta pamoja wadau kutoka taasisi mbalimbali za serikali na kiraia wakiwemo mahakimu, waendesha mashtaka, Polisi Dawati, viongozi wa dini, wanamtandao wa kupinga udhalilishaji na maafisa ustawi wa jamii.