APR ya Rwanda imetua jana Dar es Salaam kwa ajili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, lakini imeridhia kiungo Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’ achezee Azam FC katika michuano hiyo.

Migi juzi alisaini Mkataba wa miaka miwili kujiunga na Azam FC na makubaliano ya awali yalikuwa aanze kazi Chamazi baada ya kuichezea APR katika Kombe la Kagame, michuano inayoanza Jumamosi Dar es Salaam.

Lakini jana APR imeridhia Migi achezee Azam FC iliyopangwa Kundi C pamoja na Malakia ya Sudan Kusini, Adama City ya Ethiopia na KCCA ya Uganda.

APR ipo Kundi B pamoja na Al-Shandy ya Sudan, LLB AFC ya Burundi, Heegan FC ya Somalia na Kundi A kuna wenyeji, Yanga SC, Gor Mahia ya Kenya, Telecom ya Djibout, KMKM ya Zanzibar na Khartoum-N ya Sudan.

Migi anakuwa mchezaji wa sita wa kigeni wa Azam kati ya saba wanaotakiwa- na wa kwanza kabisa mpya kusajiliwa msimu huu. Wachezaji wa kigeni waliopo Azam FC ni beki Serge Wawa Pascal, kiungo Kipre Michael Balou, mshambuliaji Kipre Tchetche wote kutoka Ivory Coast, winga Brian Majwega kutoka Uganda na mshambuliaji Didier Kavumbangu wa Burundi ambao wote walikuwepo msimu uliopita.

Lakini pia, kuna wachezaji wengine wanne wa kigeni wanawania kusajiliwa Azam FC katika nafasi moja iliyobaki, ambao ni makipa Nelson Lukong kutoka Cameroon, Vincent Atchouailou de Paul Angban kutoka Ivory Coast, kiungo Ryan Burge kutoka Uingereza na mshambuliaji Allan Wetende Wanga kutoka Kenya.

Lukong na Wanga wamegoma kufanya majaribio na kocha Muingereza Stewart Hall amesema hatasajili mchezaji ambaye hajamuona mazoezini- hivyo nafasi hiyo inaweza kuchukuliwa na Burge anayaendelea na majaribio, kwani hata kipe mwingine Angban anaonekana wa kawaida.

Awali, Azam FC ilisajili wazalendo tu wawili ambao ni kiungo Ramadhani Singano ‘Messi’ kutoka Simba SC na Ame Ali ‘Zungu’ kutoka Mtibwa Sugar.

Mchezaji Mtanzania Mwingine Apata Dili Ujerumani
Kingunge: Kamati ya Maadili CCM haina maadili