Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema amepanga ratiba ya kukamilisha kutatua kero za migogoro Dar es Salaam.
Lukuvi ameyasema hayo Bungeni Dodoma katika Kikao cha Sita cha Mkutano wa pili wa Bunge 12 wakati akijibu swali la Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima la kutaka kujua mpango wa Serikali kutatua migogoro ya ardhi katika jimbo la Kawe.
“Nataka kukuhakikishia mheshimiwa Gwajima, tukimaliza Bunge hili, nimepanga ratiba ya kwenda kukamilisha kero za migogoro ya Dar es Salaam, nitatatua tatizo la Chasimba, Chatembo, Chachui, tutakwenda pamoja, na kero zote wananchi mnaoishi huko nataka mjue kwamba nitakuja na mheshimiwa Mbunge Askofu Gwajima kuhakikisha kwamba jambo hili sasa linaisha,” amesema Lukuvi.
Aidha Lukuvi amempongeza Gwajima kwa kulifuatilia suala la migogoro ya ardhi katika jimbo la Kawe hata kabla ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la Kawe.
“Nimpongeze sana Mheshimiwa mbunge wa Kawe, Askofu Gwajima, Mimi Askofu Gwajima nilikuwa simjui, lakini amenitafuta kwa shughuli hizi za kero za wananchi wa Kawe, hata kaba hajawa Mbunge, ilinilazimu kutoka kwenye kampeni kuacha kampeni zangu Isimani kwenda kumsikiliza Dar es Salaam kwa sababu ya hili” ameongeza Lukuvi.