Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi amesema kuwa anataka kuweka rekodi kwa kuifikisha timu hiyo katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa muda mrefu.

Young Africans kwa mara ya mwisho walicheza hatua hiyo mwaka 1998 ikiwa ni miaka 25 iliyopita, na sasa inataka kuweka rekodi ya kufikia hatua hiyo.

Young Africans Jumamosi (Septemba 16) wanatarajiwa kushuka ugenini nhini Rwanda kuvaana na Al Merreikh ya Sudan katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Pele.

Huo ni uwanja wa nyumbani wa Al Merreikh kutokana na nchini kwao kutokuwa na hali ya kiusalama.

Katika mchezo wa raundi ya awali, Young Africans waliifungisha virago Asas kutokea nchini Djibouti kwa jumla ya mabao 7-1, huku pia walkiwa na mwenendo bora kwenye Ligi Kuu Bara ambapo wanaongoza msimamo na pointi zao sita walizokusanya kwenye michezo miwili ya kwanza, wakifunga mabao 10, hawajaruhusu nyavu zao kutikiswa.

Akizungumza jijini Dar es salaam Gamondi amesema wanaendelea na maandalizi ya mwisho ya michezo ya hatua ya mtoano, anafahamu msimu uliopita waliondolewa katika hatua kama hiyo na Al Hilal ya Sudan.

Amesema anajua ni muda mrefu Young Africans haijacheza hatua ya makundi hali ambayo kuna ugumu na umuhimu kuwa makini katika mnichezo miwili dhidi ya Al Merreikh ya Sudan ili kufikia hatua hiyo.

“Tumejipanga kuwa na rekodi na historia mpya msimu huu, malengo yetu ni kuhakikisha tunafuzu makundi na kufika mbali zaidi, kwani tunaamini kwenye ubora wa kikosi tulichonacho.

“Tunatakiwa kuwa makini kushinda mechi zote mbili dhidi ya Al Merreikh, ugenini na nyumbari ili tuendelee kusonga mbele na mnashindano, tukipoteza tutakuwa katika hali mbaya, sitaki kuliona hilo,” amesema Gamondi.

Amesema amefanikiwa kuona baadhi ya video za mechi walizocheza Al Merreikh amefanyia kazi ubora na udhaifu wa wapinzani wao, anatambua itakuwa mechi ya ushindani kwa sababu ya rekodi ya mechi ya msimu uliopita kuondolewa na Al Hilal kutoka Sudan.

Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe, kikosi kimeingia kambini jana Jumatatu (Septemba 11) kwa wachezaji waliokuwa katika majukumu ya timu zao za taifa kasoro wachezaji wawili akiwamo Diara na Stephena Aziz Ki.

“Benchi la ufundi chini ya Gamondi limefanyia kazi ubora wa wapizani wetu, AI Merreikh ni timu nzuri na tukumbuke msimu uliopita timu kutoka ukanda wa Sudan walitutoa katika mashindano hayo na kwenda kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, sasa hivi ukiondolewa katika haya mashindano ndio umeaga,” amesema Kamwe.

Jurgen Klopp: Siwezi kuondoka Liverpool
Paul Pogba: Nilitamani kustaafu soka