Mzozo unaomkabili wakili na mwanaharakati mzaliwa wa Kenya, Miguna Miguna, umeendelea kwa siku ya pili sasa baada ya maafisa idara ya uhamiaji kumpelekea fomu za maombi ya uraia wa Kenya katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, lakini amekataa kujaza fomu hizo.
Wakili wa mwanaharakati huyo, Cliff Ombeta, amesema Miguna, ambaye amezuiliwa kwenye uwanja huo tangu alipowasili nchini hapo jana, alipelekewa fomu hizo na maafisa wa idara ya uhamiaji, baada ya kukataa kuwasilisha cheti chake cha kusafiria.
Gazeti la Daily Nation limeripoti kwamba kufikia alasiri ya leo saa za Kenya, hatima ya Miguna bado haikuwa ikijulikana na kwamba bado yuko kwenye uwanja wa ndege.
Idara ya uhamiaji ya Kenya inasisitiza kwamba Miguna alipoteza uraia wake mwaka wa 1988 alipochukua uraia wa Canada kwa sababu wakati huo, katiba ya Kenya haikuruhusu uraia pacha.
Jumanne, idara hiyo ilitoa taarifa iliyosema kwamba ni sharti aombe upya uraia huo kwa mujibu wa sheria.
Afisa mwandamizi wa idara hiyo, Joseph Munywoki, alithibitisha kwamba maafisa wake walikuwa wamempelekea Miguna fomu za kuomba uraia na alikataa kujza fomu hizo.