Mwanasiasa wa upinzani nchini Kenya aliyemuapisha kiongozi wa upinzani, Raila Odinga kuwa ‘Rais wa Wananchi’ mwezi Januari, Miguna Miguna amefukuzwa tena kutoka nchini humo.
Miguna ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba ameamka na kujikuta yuko Dubai na kwamba anahitaji matibabu.
Amesema kuwa anafahamu kwamba kuna mpango wa kumpeleka London nchini Uingereza lakini anataka kupanda ndege ya kurejea Nairobi pekee.
Aidha Mwanasiasa huyo amesema kuwa amesindikizwa kutoka Nairobi hadi Dubai na afisa wa idara ya ujasusi ya nchini Kenya.
Serikali imechukua hatua hiyo licha ya kuwepo kwa maagizo ya mahakama ya kuzuia kutimuliwa kwake na ya kuitaka serikali kufanikisha kurejea kwake nchini humo.
Hata hivyo, Idara ya Uhamiaji ya Kenya imesema kuwa Miguna alipoteza uraia wa Kenya mwaka 1998 alipopewa uraia wa Canada wakati ni kinyume cha sheria za Kenya kwa kuwa na uraia wa nchi mbili.