Mwanasheria na mwanasiasa nguli wa Kenya, Miguna Miguna amemvaa kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha ODM, Raila Odinga kwa madai kuwa amekuwa dikteta.
Miguna ambaye yuko Canada alikopelekwa kwa nguvu na Serikali ya nchi hiyo, amedai kuwa Odinga amekuwa akifanya maamuzi kidikteta kwenye chama chake na hata kwenye muungano wa vyama vya upinzani wa NASA na kwamba anataka neno lake liwe kama amri kumi za Mungu ndani ya chama.
“Hataki mfumo ambao utahamasisha uwezo, uwajibikaji kuwa ndio msingi halisi wa uongozi,” alisikika Miguna kwenye kipande cha sauti iliyosambaa mitandaoni.
Aidha, alidai kuwa ingawa alisimama na Odinga wakati wa kuapishwa kwake kuwa ‘Rais wa Wananchi’, kiongozi huyo wa upinzani amemtupa wakati ambapo anamhitaji zaidi akiwa kwenye changamoto ya kukataliwa kuingia nchini humo.
“Raila amefanya nini? Anaongea kama vile alikuwa ameshikiliwa pamoja nami! Alikuja Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta akiwa amelewa na hakuwa anaweza hata kuzungumza neno. Hakuwa na uwezo hata wa kusimama kwa miguu yake miwili,” alisema Miguna.
Mwanasheria huyo anaamini kuwa Odinga angeweza kutumia nafasi yake kuishinikiza Serikali kumrejesha nchini lakini hakufanya hivyo.
Aidha, alikosoa uamuzi wa Odinga kushikana mkono na Rais Uhuru Kenyatta na kutangaza kumaliza tofauti zilizokuwepo kati yao. Alisema hilo ni tendo la muda ambalo halitadumu na halitatua matatizo ya msingi ya hali ya kidemokrasia nchini humo.
Kwa upande wa Raila Odinga, akizungumza juzi kwa mara ya kwanza kuhusu sakata la Miguna, alimtaka mwanasheria huyo kama adui yake kwa sasa akieleza kuwa alimpigia simu na kumtaka arejee nchini, ikiwa ni sehemu ya makubaliano yake na Rais Kenyatta.
Hata hivyo, alimlaumu mwanasheria huyo kwa kukataa kushirikiana na maafisa wa Uhamiaji kukamilisha taratibu za kurejea nchini na badala yake kuanza kumshambulia kwa maneno.
Miguna ambaye alisimamia zoezi la kumuapisha Odinga, aliondolewa kwa nguvu nchini Kenya kuelekea Canada. Alirejea kimyakimya lakini alizuiliwa uwanja wa ndege kwa siku tatu kabla ya kurejeshwa tena kupitia Dubai.