Maafisa wa Jeshi nchini Libya, wamesema wamegundua miili 42 isiyojulikana kwenye kaburi la pamoja jirani na shule ya Ibn Khaldoun, iliyopo eneo la Jiza al-Bahriya kaskazini mwa nchi hiyo, iliyopelekwa hospitali kuchukua sampuli za mifupa na kuzikwa baadaye baada ya matokeo ya kitabibu.
Maafisa hao, kupitia mamlaka ya Jumla ya Utafiti na Utambulisho wa Watu Waliopotea, wamesema walipokea taarifa kutoka kwa ofisi ya mwendesha mashtaka wa eneo hilo, kuhusu kaburi la pamoja lililopatikana katika shule hiyo ya mji wa pwani wa Sirte ambayo ilitolewa kwa muda wa wiki mbili za kazi.
Wamesema, “Sampuli zilichukuliwa kutoka kwa mifupa kwa uchambuzi wa DNA, kwa uratibu na ofisi ya uchunguzi, na inasadikika haikuwa rahisi kugundua eneo hilo kwakuwa lilikuwa likilindwa na wanajihad ambao hawakutaka mtu asogee mahala hapo kiurahisi na walipoondoka watu wakataka kufahamu kilichopo.”
Wanajihadi hao wenye itikadi kali, walikuwa wamelinda jiji hilo vikali kwa miezi kadhaa, kwa kutumia mbinu za waasi wa mijini kabla ya kushindwa na vikosi vinavyoiunga mkono serikali mwishoni mwa 2016 huku miili hiyo ikisadikiwa kuwa ya watu waliouawa na kundi la kigaidi la Daesh/ISIS ambalo liliuteka mji huo kwa zaidi ya mwaka mmoja kuanzia Agosti 2015 hadi Disemba 2016.
Ugunduzi wa makaburi ya halaiki, ni jambo la kawaida katika nchi ya Libya iliyokumbwa na vita, haswa katika mji wa Tarhuna, ambao ulikuwa ngome ya mbabe wa kivita Khalifa Haftar na hivi majuzi, makaburi mawili ya halaiki ya miili saba na nane mtawalia yaligunduliwa katika ua wa hospitali, huko Sirte mwishoni mwa mwezi Agosti 2022.
Kulingana na vyanzo rasmi vya Libya, vikosi vya Haftar na wanamgambo washirika walifanya uhalifu wa kivita na vitendo vya mauaji ya kimbari, kati ya Aprili 2019 na Juni 2020.