Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tunisia, Kamel Feki amesema miili 901 ya Wahamiaji waliokufa maji katika pwani ya nchi hiyo imepatikana kuanzia Januari 1 hadi Julai 20, 2023.
Taifa hilo la Afrika Kaskazini linashuhudiwa kuwa na wimbi kubwa la uhamiaji mwaka huu, huku majanga ya mara kwa mara ya kuzama kwa maboti ya wahamiaji kutoka nchi za Afrika, Kusini mwa jangwa la Sahara wakielekea kwenye pwani za Italia yakitukia.
Tunisia, imechukua nafasi ya Libya kama kituo kikuu cha kuanzia safari kwa watu wanaokimbia umaskini na mizozo barani Afrika na Mashariki ya Kati, kwa matumaini ya kuwa na maisha bora barani Ulaya.
Feki aliliambia bunge kuwa miongoni mwa miili hiyo 901 iliyopatikana, 36 ilikuwa ya Watunisia na 267 ya wahamiaji wa kigeni, huku uraia wa waliobaki ukiwa haujulikani.