Baadhi ya miili ya watu waliouawa Ijumaa iliyopita nchini New Zealand katika tukio la kufyatuliwa risasi kwenye misikiti miwili na mtu mmoja ambaye ametajwa kuwa mbaguzi, imeanza kutolewa kwa ndugu.
Jeshi la polisi nchini humo limesema kuwa uchunguzi wa miili hiyo umekamilika lakini ni miili 12 tu ndio wametambuliwa rasmi, na kwamba katika kundi hilo, sita imeshakabidhiwa kwa wana familia.
Aidha, katika taarifa iliyotolewa na polisi katika mji wa Christchurch imesema kuwa wakati utambuaji wa miili ukionekana kuwa ni rahisi, ukweli ni kwamba umekuwa mgumu hasa katika hali kama hiyo.
Waziri mkuu wa nchi hiyo, Jacinda Ardern amesema kuwa kufikia Jumatano wiki hii, miili yote itakuwa imekabidhiwa kwa familia husika.
Siku ya Jumamosi mtu anayeshukiwa kuwa na itikadi za mrengo wa kulia, Brenton Tarrant, alifikishwa mahakamani nchini New Zealand kufuatia mashambulizi hayo, yaliyofanyika mjini Christchurch.
Tarrant, mwenye umri wa miaka 28 ambaye ni raia wa Australia, akiwa amefungwa pingu alisimama kimya mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Christchurch kabla ya kurudishwa rumande bila ya kusema chochote.