Hali ya mvutano imezidi kuongezeka kati ya utawala mpya wa Kijeshi wa Niger na Jumuiya ya ukanda wa Afrika Magharibi – ECOWAS, ambayo imekuwa ikiratubu utumaji wa vikosi vya Wanajeshi kurejesha demokrasia nchini humo huku Wanajeshi waliopindua nchi wakisema watamuuwa Mohamed Bazoum ikiwa watazidi kufuatiliwa.
Mapema Agosti 10, 2023 ECOWAS ilisema imeamua kupeleka kikosi kinacholenga kurejesha utaratibu wa kikatiba nchini Niger, baada ya muda wa masharti yake ya kumrejesha madarakani Rais aliyepinduliwa, Mohamed Bazoum kumalizika.
Rais wa Niger, Mohamed Bazoum aliyeondolewa madarakani kijeshi.
Hapo jana, Agosti 12, 2023 Maafisa wawili wa nchi za Magharibi walisema utawala wa Niger ulimwambia Mwanadiplomasia Mkuu wa Marekani kwamba wangemuua Bazoum, ikiwa nchi jirani zitajaribu kuingilia kati kijeshi kurejesha utawala wake.
Hata hivyo, bado haijulikani siku ya kupelekwa kwa kikosi cha ECOWAS, na jinsi ripoti za vitisho dhidi ya Bazoum zingeathiri uamuzi wa jumuiya hiyo yenye wanachama 15 kuingilia kati, huku ikidaiwa kikosi hicho kinaweza kuwa na wanajeshi 5,000 wakiongozwa na Nchi ya Nigeria.